Wednesday, November 29, 2017

Uchawi

UCHAWI


NINI MAANA YA UCHAWI?

Al Azhari ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya kiarabu iitwayo “LisanulArab” amesema:
“Neno “Uchawi”, kwa kiarabu “As Sihr”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na Shaytwaan na kwa msaada wake (Shaytwaan)”, na akasema pia kuwa; “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli.”
Ama Swahaba Ibni 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki."
Hayo ni katika kamusi za lugha.

Amma katika kamusi ya dini, maana ya neno Uchawi (As Sihr), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Al Razi kuwa;
"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)."
Amma Shaykh Wahiyd Abdulsalaam Bali, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'Al Saarim Al Batar fiy muhaarabat Al Saharatul ashraar', na kitabu kiitwacho "Al wiqaya mina l jinni wa shaytan", ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika elimu ya majini na Mashaytwaan na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:
"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kwa kila anachotaka."

Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na Shaytwaan ayatende ili ajikurubishe naye ni:

 Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni
 Aandike baadhi ya aya za Qur-aan kwa damu ya hedhi.
 Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aya za Qur-aan penye nyayo za miguu.
 Au aiandike suratulFatiha kinyume nyume.
 Asali bila ya Udhuu.
 Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la Allaah kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na Shaytwaan.
 Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia.
 Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake

Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama.
Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajji akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji.
Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy.

Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi ende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.
Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa akenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.
Yule kijana alishtuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia:
"Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?"
"Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."
Yule kijana akajibu:
"Mimi ninamsujudia Allaah peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia."
Ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jini yule.

Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake atumikiwe kwa kutendewa matendo ya kufru, na maulamaa wanasema:
"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi Shaytwaan humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majini au kwa kiarabu wanaitwa "Maradatul Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi, na kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi."
Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na Shaytwaan ni marafiki na washirika katika kumuasi Allaah.

Allaah Anasema:
"Na (wakumbushe) siku atakapowakusanya wote (akawaambia): "Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu". Na marafiki wao katika wanaadamu (watagombania) waseme:  "Mola wetu! Tulinufaishana sisi na wao na tumefikia muda wetu uliotuwekea". Basi (Allaah) atasema; "Moto ndio makazi yenu, mtakaa humo milele", ila apende Allaah (kuwarehemu), hakika Mola wako ndiye Mwenye hikima (na) ndiye ajuaye.”
Al-An'aam - 128

No comments:

Post a Comment

SHEIKH SHARIF YUSSUF

HASAD KATIKA NDOA 1

HASAD KATIKA NDOA:  Baadhi ya watu hufanya chuki ama husda katika ndoa za watu kwa kutumia vitu mbalimbali, ikiwa kwa kusambaza maneno ya k...