Sunday, December 24, 2017

HASAD KATIKA NDOA 1

HASAD KATIKA NDOA:
 Baadhi ya watu hufanya chuki ama husda katika ndoa za watu kwa kutumia vitu mbalimbali, ikiwa kwa kusambaza maneno ya kuharibu kwa watu wa nje, ama familia ya mume au mke, wengine hufikia kutumia mpaka njia za kishirikina kwa lengo la kutaka kutafarakanisha (kuachananisha) ndoa za watu, sio wanadamu tu ambao hufanya uhasidi katika ndoa bali pia wapo hata majini ambao huleta mifarakano katika ndoa,husababisha ndoa za watu kuharibika.
BAADHI YA DALILI ZA NDOA ZILIZOHUSUDIKA:
   Zifuatazo ni dalili za ndoa ambazo zilizohusudika kwa namna mbalimbali ambazo husababishwa na maneno (fitna),ama kwa kutumiliwa njia za kishirikina zinazofanywa na binaadamu.
(1)"kuona mtu ambae huchukia  neema ambazo Allah (سبحنه وتعلى) amekuruzukuni katika ndoa yenu "
(2)"Kuona mtu ambae hufatilia na kutaka kuyajua yale ambayo yamo mpaka ndani ya ndoa yenu"
(3)"Ikiwa umekhitalifiana na mtu akawa ana kutishia amani katika ndoa yako"
(4)" Hata kuona mabadiliko kwa Mume/Mke ambayo ya sio mazuri na yaliyokuja kwa ghafla bila sababu kuijua"
(5)"Ikitokea umekhitalifiana (umekoseana) na mwanandoa mwenzako kwa khitilafi ndogo sana na ukaona ugomvi ni mkubwa bila ya kutarajia ugomvi huo kuwa itatokea kwa namna hiyo"
    Hizi ni baadhi ya dalili za ndoa ambazo zilizohusudika, ama  kwa baadhi ya dalili ambazo zinazosababishwa na  majini ni hizi zifuatazo.
BAADHI YA DALILI AMBAZO HUSABABISHWA NA MAJINI KATIKA KUTAFARAKANISHA NDOA:
(1)"Ikitokea kwa Mume kukosa nguvu wakati  watendo la ndoa na kujikuta usiku anapata ndoto za kufanya mapenzi na binti na akawa na nguvu".
(2)"Mke kukosa ladha ama utamu wa tendo kila unapofanya tendo la ndoa Mume"
(3)"Mume/Mke kutokuwa na hamu ya kuwa karibu na mwenzako kila mara"
(4)"Mume/Mke kuwa na hasira za ajabu ajabu kila unapokuwa na mwenzako"
(5)"Mme/Mke kuota kila mara ndoto za kufanya mapenzi".
    Hizi  ndio baadhi ya dalili ambazo husababishwa na majini ambao huleta husda katika ndoa, nini upi utatuzi wa matatizo haya.
UTATUZI:
     Ukiona matatizo haya yanakusibu kwa namna moja ama nyengine kinachotakiwa ni kumuelekea Mungu kwa kufanya dua za kumuomba yeye kuweza kukukinga na pia kukuondoshea haya matatizo, zipo dua mbalimbali za kufanya kumuomba Allah (سبحنه وتعلى) na akakuondoshea shida hizi ulonazo.
Ama wasiliana nasi ili tuweze kukusaidia kwa uwezo wa Allah(سبحنه وتعلى)
WASILIANA NASI
No:     +255676457532
Email:Alruqiyyatulshariyyah@gmail.com
           Yussufmohammed360gmail.com
Insta: sheikh_sharif_yussuft
You:   sheikh sharif yussuf
Blog:  sheikhsharifyusuph.blogspot.com

Monday, December 4, 2017

Umuhimu wa aqiyda


Chanzo: ‘Aqiydah (Mambo ya Iymaan) Kwanza ...Laiti Kama Wangalijua


Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaarifu Mu’aadh bin Jabal, wakati alimpomtuma kwenda nchi ya Yemen, “Wewe unakwenda kwa watu Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitaab) Basi jambo la kwanza kuwalingania liwe kumuabudu Allaah. Kama wakilikubali hilo, ndio kisha uwataarifu kwamba Allaah amewajibishia juu yao sala tano wakati wa usiku na mchana.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Hadiyth hii iko wazi kabisa. Na haihitaji maelezo mengi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katumia kanuni hii katika uilinganizi wake wa kuwaita watu ndani ya Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa katika mji wa Makkah kwa muda wa miaka kuminatatu akiwafunza watu iymaan na kuwaelimisha Maswahaba zake juu ya nukta hii na kusahihisha iymaan za watu. Huu ndio mfumo waliokuzwa nao Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). 

Jundub bin ‘Abdillaah Al-Bajaliy akasema, “Tumejifunza iymaan na kisha tukajifunza Qur-aan nayo ikatuongezea iymaan yetu.”

'Abdullaah bin ‘Umar alisema, “Sisi tuliishi wakati ambapo mmoja wetu atafunzwa iymaan kwanza kabla ya kufunzwa Qur-aan na wakati Surah zikiteremka tulijifunza ni nini kilichoruhusiwa na nini kilichopigwa marufuku na kipi kilichokatazwa na kipi kilichoamriwa na upi unapaswa kuwa msimamo wetu juu yao. Lakini nimeona watu wengi waliofunzwa Qur-aan kabla ya iymaan. nao huisoma kutoka mwanzo wa Kitabu hadi mwisho wake pasi na wao kufahamu nini imeamrisha na nini imekataza na bila ya kuufahamu msimamo wao juu yake. Anakuwa kama mtu ambaye anayezitupa tende (yaani, hafaidiki na kuisoma kwake Qur-aan)."

Hiyo ndio njia ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyowaleya nayo Maswahaba wake: Iymaan kwanza kisha Qur-aan.
Hii ni sawa na kile Imaam Abu Haniyfah alichosema: “Elewa Dini kwanza (yaani Tawhiyd) kisha ndio uelewe sayansi yake (yaani Shari'ah).”

Iymaan lazima isahihishwe kwanza, kisha ndio yafuate mambo mengine ya Dini.

Na Imaam Ash-Shafi'iy akasema, “Yakuwa ni bora mja akutane na Allaah kwa kila aina ya dhambi isipokuwa shirki kuliko kukutana na Allaah hali ya kuwa amezusha jambo katika Dini.”

Neno Al-‘Aqiydah asili yake imetokana na neno ‘aqada. Katika lugha ya Kiarabu, panasemwa, “Aqada Al-Habl” kumaanisha wakati kamba imefungwa imara. Na, “’Aqada Al-Bay’” (Mkataba wa Mauzo)” au “Makubaliano ya bei” wakati mtu anapoidhinisha mkataba wa mauzo au makubaliano. Na Allaah Anasema katika Qur-aan,

“Na wale ambao mmefungamana nao ahadi (‘aqadat), basi wapeni sehemu yao.” [An-Nisaa: 33].

Na vilevile Allaah Anasema,

“Allaah Hatokuhisabuni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuhisabuni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mliyoifunga thabiti (‘aqadtum).” [Al-Maaidah: 89].

“Na timizeni Ahadi ya Allaah mnapoahidi, na wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha." [An-Nahl: 91].

Mfano wa mtu kusema ‘Aqadtu juu ya jambo ni kumaanisha yakuwa moyo wake umekita juu ya hicho alichokidhamiria.

Kwa hiyo, Al-‘Aqiydah au Al-I’tiqaad kulingana na Wanachuoni wa Kiislamu ni: iymaan imara iliyokita ndani ya moyo wa mtu pasi na kutetereka au kuwa na shaka yoyote. Na inaoondosha dhana, shaka au wasiwasi.

Imaam Abu Haniyfah kaliita somo hili adhimu Al-Fiqh Al-Akbar (Ufahamu ulio Adhimu) na ndio ufahamu wa Dini. Aliita sayansi ya shari’ah; ufahamu wa sayansi.
Wanachuoni wengi wa Kiislamu hulitumia neno Tawhyid kwa mambo yote ambayo mtu lazima ayaamini. Hii ni kwa sababu kilicho muhimu zaidi katika mambo yote ni msingi wa Tawhyid uliomo ndani ya maneno, “Hakuna anayestahili kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah (Shahaadah).”

Tawhiyd, kulingana na wao, inaweza kugawanywa katika makundi mawili: Tawhiyd ya utambuzi na uthibitisho na Tawhiyd ya makusudio na matendo.
Tawhiyd ya utambuzi na uthibitisho ni Tawhiyd ya Upweke wa Muumbaji na Tawhiyd ya Majina Yake na Sifa (yaani Yeye ni Mpweke na Ndie Muumba na ni Mpweke katika Majina na Sifa Zake).
Tawhiyd ya makusudio na matendo ndio Tawhiyd ya Uuluwhiyyah yaani hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah (yaani, Yeye Pekee tu Ndiye Anayestahili kuabudiwa).

Wanatheolojia ‘Kalaamiyyuwn’ - na nini kitachokujuza wewe hao wanatheolojia ni wepi? – Wameliita somo hili adhimu “mzizi wa dini” na wakaiita shari’ah “matawi ya dini.” Hii ni istilahi yao. Sisi hatuafikiani nao katika jambo hili lakini hapa si pahala pake pa kulijadili. Wote wameipatia jina au kivumishi kulingana na mahitaji yao.
Lakini ni jina gani Qur-aan imelipa jambo hili?
Qur-aan imeliita jambo hili kwa jina la Iymaan. Allaah Anasema katika Qur-aan:
Na hivyo ndivyo Tulivyokufunulia (Wahyi) kwako roho katika Amri Yetu. Hukuwa unaelewa nini Kitabu, na wala (nini) Iymaan, lakini Tumeijaalia (kuwa) Nuru, Tunamhidi kwayo Tumtakaye kati ya waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kwenye Swiraatwim-Mustaqiym  (njia iliyonyooka).” [Ash-Shuwraa: 52]

Kwa ujumla moyo wa Muumin lazima uwe thaabit kuhusu “nguzo” hii ya iymaan. Lakini mtu hatoitwa Muumin tu kwa kujua na kuelewa nguzo hizi lakini ni lazima aridhiye na atekeleze kile kinachoelezewa, katika Hadiyth ya Jibriyl, kama ndio Uislamu. Iymaan, kwa namna hii, inajumuisha Uislamu.

Kama Iymaan ingekuwa inatosha kwa mtu kujua ukweli katika moyo wake tu, basi kuna tofauti gani baina yake na shaytwaan au Fir’awn (Kumbuka: Shaytwaan alikuwa mwenye elimu kubwa juu ya Mola wake lakini aliangamizwa kwa sababu ya kiburi chake na wivu. Na Fir’awn, ingawa yeye alidai Uungu, alijua kwamba Mungu wa kweli  ni Allaah na kwamba hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Yeye. Allaah Anasema:

“(Muwsaa) Akasema: “Kwa yakini umekwishajua kwamba hakuna Aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi kuwa ni dalili za kuonekana dhahiri.” [Al-Israa: 102]. - Ingawa walijua ukweli, hawakukubali kuielekeza ‘ibaadah yao kwa Allaah Pekee).

Katika Hadiyth ya Jibriyl, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alielezea nguzo za hii iymaan ambayo kila mwanaadamu lazima aamini, na alipoulizwa, “Ni nini Iymaan?”, Alisema, “Ni kumuamini Allaah na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Wake na Siku ya Mwisho na Kheri na Shari vyote vinapatikana kwa Qadari ya Allaah.”

Ni lazima kwa kila mtu kuzijua nguzo hizi na kujifunza ufahamu ulio sahihi na kuamini katika ufahamu wa wema wetu waliotangulia walivyofahamu na kuamini, kwa namna walivyofahamu wao kutoka kwa Maswahaba wa Mtume  (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wale wote waliowafuata katika njia hiyo. Hii inajumuisha pamoja na ma-Imaam wanne, na Sufyaan Ath-Thawriy, Sufyaan bin 'Uyaynah, ‘Abdullaah bin Al-Mubaraak na wengine sawa na wao, kama vile Muhammad bin Isma’iyl’ Al-Bukhaariy, Muslim bin Al-Hajjaaj, Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah na Al-Haafidhw Ibn Al-Qayyim. Na Wanachuoni wote walio sawa nao katika ufahamu ambao waliofuata mwenendo  ule ule katika kufahamu na kuziamini nguzo hizi.

Huu ni wajibu wa kwanza juu kiumbe mwenye dhima. Hakuna tofauti ya maoni juu ya suala hili miongoni mwa wasomi ambao maoni yao yanastahiki kufuatwa. Imaam Abu Haniyfah kasema: “Kuelewa iymaan ni bora kuliko ufahamu wa sayansi.” Alichokusudia katika usemi huu kuwa; Iymaan ni Tawhiyd na sayansi ni Shari’ah. Kwa hiyo katanguliza ufahamu wa Tawhiyd kabla ya mtu kufahamu Shari’ah.

Na Shaykh Al-Islaam Al-Haruwi Al-Answaariy (Aliyefariki 481 H) amesema katika mwanzo wa kitabu chake ‘I’tiqaad Ahl As-Sunnah’“Wajibu wa kwanza juu mja ni maarifa juu ya Allaah. Hii inathibitishwa na Hadiyth ya Mu’aadh, wakati alipoambiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Wewe unakwenda kwa watu Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitaab) Basi jambo la kwanza kuwalingania liwe kumuabudu Allaah. Kama wakilikubali hilo, ndio kisha uwataarifu kwamba Allaah amewajibishia juu yao sala tano wakati wa usiku na mchana.” [Al-Bukhaariy na Muslim]


Kutokana na  uadhimu wa nguzo hii ndio Maulamaa wakubwa wa Kiislamu wameitanguliza. Tafakari, kwa mfano, kile Imaam Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy alivyofanya katika kitabu chake Al-Jaami’ Asw-Swahiyh, ambayo ni kitabu sahihi zaidi baada ya Kitabu cha Allaah, Utaweza kuona kwamba kutokana na elimu yake ya kina na ufahamu wake wa Dini hii. Imaam huyu mkubwa alianza kitabu chake kwa “Mwanzo wa Ufunuo” na kisha ikifuatiwa na mlango juu ya iymaan, na kufuatiwa na mlango juu ya maarifa. Kama kwamba alikuwa akimaanisha (Allaah Amrehemu), kwa uhakika wajibu wa kwanza juu ya mwanaadamu ni iymaan na njia ya kuifikia iymaan ni maarifa. Na chanzo cha iymaan na maarifa ni ufunuo. Hivyo, alianza kwa kuonyesha jinsi ufunuo ulivyotokea na namna ulivyokuwa. Kisha akafuatia kutaja iymaan na maarifa. Utaratibu huu si ajali; na kwayo ametutengenezea baadhi ya nukta muhimu.

Hii ni jumla ya kile ambacho tunataka kukutaarifuni na kwayo ndio tunapaza sauti zetu juu. kipaumbele cha kwanza ni suala la ‘Aqiydah. Iymaan na maarifa ni njia ya kuifikia. Na chanzo cha maarifa na iymaan ni Kitabu na Sunnah.

Friday, December 1, 2017

01-Ruqyah Ya Shariy'ah Na Hukmu Zake

Maradhi  na  madhara yoyote yale hayamsibu mtu isipokuwa kwa majaaliwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini kwa rahmah Yake ‘Azza wa Jalla, Amejaalia shifaa (poza) kwa kila maradhi na kila dhara, kwa kutumia ruqyah pamoja na tiba ya Sunnah, na pia kutokana miti na majani kadhaa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amejaalia kuwa ina tiba ndani yake kwa dalili:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَا أَنْزَلَ اللَّهُ دَاءً إِلاَّ أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً)) رواه البخاري   
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Hakuteremsha maradhi isipokuwa Ameyateremshia shifaa)) [Al-Bukhaariy]

Pia:
وعَنْ جَابِرٍعَنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم؛ أَنَّهُ قَالَ: ((لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءٌ، فَإِذَا أُصِيبَ دَوَاءُ الدَّاءِ بَرَأَ بِإِذْنِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ)‏) رواه مسلم  
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuna dawa kwa kila maradhi, na pindi dawa inapotumiliwa katika maradhi huponyesha kwa idhini ya Allaah ‘Azza wa Jalla)) [Muslim katika Kitaab As-Salaam

Pia:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مَسْعُدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يُنْزِلْ دَاءً إلاَّ  أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ، وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ))
Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla) Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha pamoja nayo shifaa, amejifunza aliyejifunza na amekuwa jahili aliyekuwa jahili kwayo)) [Musnad Ahmad (6/121) kwa isnaad Swahiyh. Taz. Majmuw’ Fataawa Ibn Baaz (1/171), (6/290)]


Imekatazwa kutumia dawa za haraam kwa dalili:

عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه)  قَالَ:  قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ اللَّهَ أَنْزَلَ الدَّاءَ وَالدَّوَاءَ، وَجَعَلَ لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءً، فَتَدَاوَوْا ولاَ تَدَاوَوْا بِحَرَامٍ))
Kutoka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake, Akajaalia kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraam)) [Abuu Daawuwd, Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy ameipa daraja ya Hasan, Taz. Takhiryj Mishkaat Al-Maswaabiyh(4/272), Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (1762) au (2390)]

Inafaa kusoma Suwrah au Aayah ambazo imepatikana dalili zake, lakini Qur-aan nzima ni shifaa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾
Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara. [Al-Israa 17: 82]

Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾
Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini. [Yuwnus 10: 57[

‘Ulamaa wamejuzisha ruqya pindi ikipatikana masharti matatu ambayo ameyanukuu Al-Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu-Allaah): 
  1. Iwe kwa maneno ya Allaah (Ta’aalaa) au kwa Majina Yake na Sifa Zake.
  2. Isomwe kwa lugha ya Kiarabu.
  3. Aitakidi kwamba si ruqya pekee ndiyo itakayomponyesha bali aitakidi kwa uwezo wa Allaah (Ta’aalaa).
Pia zifutazo ni nukta muhimu Muislamu azingatie kabla ya kufanya ruqyah:

1-Uitakidi moyoni mwako kwamba njia yoyote uitumiayo ikiwa ni ruqyah, au kutumia dawa, hakupatikani shifaa isipokuwa kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwa hiyo uanze kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee ili Akutakabalie ruqyah yako.


2-Unaweza kutumia Aayah na du’aa za Qur-aan na Sunnah madamu tu hutozitumia kwa kuziwekea idadi maalumu, au wakati maalumu ambavyo haikupatikana dalili, au kutumia njia nyinginezo kama kuweka kwenye hirizi, au kutundika mahali n.k. ambapo itakuingiza katika shirki. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya hayo aliposema: 

عَنْ عَوْفِ بْنِ مَالِكٍ الأَشْجَعِيِّ قَالَ: كُنَّا نَرْقِي فِي الْجَاهِلِيَّةِ فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ، كَيْفَ تَرَى فِي ذَلِكَ؟ فَقَالَ: ((اعْرِضُوا عَلَيَّ رُقَاكُمْ لاَ بَأْسَ بِالرُّقَى مَا لَمْ يَكُنْ فِيهِ شِرْكٌ))
Kutoka kwa ‘Awf bin Maalik Al-Ashja’iyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Tulikuwa tunafanya ruqyah katika zama za jahiliyyah, tukasema: Ee Rasuli wa Allaah,  unaonaje katika hayo (ruqyah yetu]? Akasema: ((Nionyesheni ruqyah yenu, hakuna ubaya katika ruqyah madamu tu haitokuwa na shirki)) [Muslim katika Kitaab As-Salaam, Abuu Daawuwd katika Kitaab Atw-Twibb]

3-Akipenda mtu, anaweza kubakia katika kutawakkal kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee bila ya kujizingua au kuomba kufanyiwa ruqyah kama ni mojawapo ya fadhila za kumuingiza mtu Jannah bila ya kuhesabiwa kama alivyosema  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفًا بِغَيْرِ حِسَابٍ: هُمْ الَّذِينَ لاَ يَسْتَرْقُونَ ولاَ يَتَطَيَّرُونَ وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ))
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wataingia Jannah kati ya Ummah wangu watu elfu sabini bila ya hesabu; hao ni wale ambao hawaombi kufanyiwa ruqyah, wala hawatabirii nuksi au mkosi, wala kujitibu kwa moto, bali wanatawakkal kwa Rabb waotu.)) [Al-Bukhaariy, Muslim]


​Tunaona kwenye Hadiyth hiyo kuwa, ni bora zaidi mtu kujizuia kuomba kufanyiwa ruqyah -  japo ni jambo lenye kuruhusiwa-, lakini ni bora zaidi kuacha kuomba kufanyiwa ruqyah na kuwa ni mwenye kutawakkal kwa Allaah, kwa sababu hiyo ni katika sababu ya kupata Pepo.


4-Ujiepushe  na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kinyume chake ni kudumisha Tawhiyd ya Allaah (kumpwekesha) kwa Ar-Rubuwbiyyah (Uola), Al-Uluwhiyyah ('Ibaadah), na Asmaa wasw-Swifaat (Majina na Sifa Zake). 

5- Ujiepushe na maasi na ubakie katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).


5-Udumishe Adhkaar za asubuhi na jioni, na Adhkaar za kulala kwa mfululizo bila ya kuacha  hata baada ya kupata tiba ili ujikinge kutokurudiwa tena kudhuriwa na viumbe viovu na shari zao.


6-Uvute subira na ukumbuke fadhila za kuvuta subira ili zikusaidie kuvumilia madhara yaliyokusibu.


7-Uanze kusoma ruqyah kwa thanaa - kumtukuza na kumsifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kufuata adabu za kuomba du’aa  ili itakabaliwe ruqyah yako.

SABABU ZILIZOSAHAULIKA ZA KUJIBIWA DUA

بسم الرحمن الرحيم
الحمد لله رب العلمين, والصلاة والسلام علي اشرف المرسلين, نبينا محمد وعلي اله وصحبه اجمعين, وبعد

Hakika ya kumuomba Mola aliyetukuka aliye juu ni katika vitendo vitukufu na vilo bora.
Amesema Mola aliyetukuka katika ubora wake:
{{Yalaiti iwajiapo adhabu wangenyenyekea kwa kuomba du’aa lakini zimekua ngumu nyoyo zao hazina imaan; Na wamepambiwa na shaytwaan kwa yale wayafanyao.}} [Al-An’aam: 43]

Na akasema Aliyetukuka:
{{Sema kuwaambia hamukukithirisha; kufanya kwa wingi; wala kuzingatia lau mungenyenyekea na kumuomba Yeye katika shida; hakika mumekanusha; mumekataa; kwanini adhabu isiwe lazima kwenu? Mwastahili kuadhibiwa.}} [Al-Furqaan: 77]
Yaani lau musingejali kwa kuomba na kufanya ‘ibaadah kwa wingi. 

Na Hadiyth iliyopokewa na at-Tirmidhiy akiisahihisha Shaykh Al-Albaaniy; amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Hakuna kitu kitukufu  kuliko du’aa; kuomba du’aa.))

Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Mwenye kutaka kujibiwa du’aa na Allaah wakati wa shida na dhiki, na azidi kufanya kwa wingi wakati wa raha zake kuomba.))[Imepokewa na at-Tirmidhy akasema Shaykh Al-Albaaniy ni Hasan]
Na imepokewa na Daylamiy kutoka kwa Anas bin Maalik amesema: Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Hamfungulii Mola mja Wake kuomba kisha akamfungia mlango wa kujibiwa, Mola ni Mtukufu hawezi kufanya hivyo.))

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Mwenye kushindwa katika watu (yaani mpungufu ama dhaifu) ni yule anayeshindwa katika du’aa (mpungufu ama dhaifu wa kuomba du’aa).)) [Imepokewa na at-Twabraaniy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]
Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Hakuna kinachorudisha hukumu ya Mola isipokuwa du’aa.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy  na akaipendezesha Shaykh Al-Albaaniy]
Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa Mola Aliyetukuka na Aliye juu, kulingana na thamani ya du’aa ya kinga aliyo hukumu Mola kwa mja Wake.

Kwa hivyo amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Du’aa yanufaisha kwa yaliyoteremka na yasiyoteremka, kutoka kwa Allaah.)) [Imepokewa na al-Haakim kutoka kwa Ibnu ‘Umar]
Na amesema Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuusisitiza Ummah wake katika kuomba kwa kila kitu: 
((Hakika ataomba mmoja wenu Mola wake haja zake mpaka uzi wa viatu vyake.)) yaonyesha hatodharau kumuomba hata kwa kitu kidogo mfano gani ataomba. [Imepokewa na at-Tirmidhiy na Ibnu Hibbaan kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu).]

Na kujibiwa kwa du’aa kuna sababu nyingi, mwenye kushikana nazo kwa uwezo wa Mola Aliyetukuka na Aliye juu ni sababu ya kuondolewa mazito yake na kutekelezewa haja zake. 

Tutazitaja sehemu katika hizo tukitaraji kwa Mola kukubaliwa na kunufaisha.
1) Du’aa uinukapo usingizini usiku ni sababu katika sababu za kujibiwa du’aa. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) zimfikie: Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: 
((Mwenye kuinuka usiku akasema laa ilaaha illa Allaah wahdahu laa shariyka lahu, lahul mulku wa lahul hamdu wa huwa ‘alaa kulli shay-in qadyr, wala hawla wala quwwata illa biLlaah, kisha  akasema  ee Mola nisamehe, ama aombe atakalo atajibiwa, na akitawadha na kuswali itakubaliwa Swalah yake.))

2) Na katika sababu ya kukubaliwa du’aa ni neno: Hakuna Mola isipokuwa Wewe, umetakasika, hakika mimi nimekuwa katika madhaalimu. Imetoka kwa Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: 
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Uombezi wa Dhannuun alipoomba naye yupo tumboni mwa samaki ni:
La ilaaha illa anta subhaanaka inniy kuntu mina dhw dwaalimiyn
Hataomba kwa du’aa hiyo Muislam yeyote kwa neno hilo ila atajibiwa du’aa yake.)) [Imepokewa na Tirmidhiy]

3) Kujiepusha na haraam katika kula kunywa na mavazi. Hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa na kutofanya hilo ni sababu ya kutojibiwa. Kwa kujivisha maasi hiyo ni katika sababu kubwa ya kutojibiwa du’aa.
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((Hakika Mola ni mzuri na hakubali isipokua mazuri... kisha akamtaja mtu aliyekuwa safarini mwake ndefu aliyejawa na vumbi, akainua mikono yake mbinguni: Ee Mola, Ee Mola, na chakula chake ni cha haraam na kinywaji chake haraam, na mavazi yake haraam na nyama yake ya mwili imekuwa kwa haraam. Vipi Mola Aijibu du’aa yake.))[Imepokewa na Muslim]
Amemuweka mbali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu huyu kuwa hatojibiwa du’aa hata akiomba vipi. Kule kuwa mbali kwake na kujibiwa du’aa ni kuwa katika haraam. 
Ameifasiri Ibn Rajab Hadiyth hii kuwa ni dalili kubwa kuwa haikubaliwi ‘amali yoyote wala haitakaswi isipokuwa kwa kula halali. Na kula haraam huharibu kitendo cha mtu na kukataza kupokelewa du’aa na Allaah Aliyetukuka.

Imepokewa na Ikrimah bin ‘Ammaar kutoka kwa Asfar kuwa amesema: Aliambiwa Sa’ad bin Abi Waqaas: Kwa nini du’aa zako katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni zenye kujibiwa? Akasema: “Sitii mdomoni kwangu tonge isipokuwa niijue imetoka wapi, na imekuja kivipi.”

Kutoka kwa Wahaab bin Manbah amesema: 
“Mwenye kutaka kujibiwa du’aa yake na Allaah, kiwe halali chakula chake.”
Fanya pupa ewe ndugu Muislam kiwe chakula chako, kinywji chako, na mavazi yako yawe halali, ili upate kujibiwa du’aa yako na uepuke na moto.

4) Kuomba kwa (kutawasali) du’aa zako kwa kuziunganisha na vitendo vyema, basi hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa.
Dalili ya hilo ni Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika swahiyh yake: Kutoka kwa Ibnu ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Walikuwa watu watatu wakitembea, ikawanyeshea mvua wakajisitiri katika pango, likafunikika mahali pa kutokea jiwe kubwa katika jabali, wakasema wao kwa wao: Angalieni vitendo vyema mulivyofanya mumuombee navyo Allaah, huenda Akatufariji. Akasema wa kwanza wao: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na wazazi wawili na mke na watoto wadogo nikiwalea, niwaendeapo na maziwa huwaanzia wazazi wangu nikawanywesha kabla watoto wangu. Nilichelewa siku moja sikuja isipokuwa usiku nikawakuta wamelala nikasimama na maziwa kwa kuchukia kuwaamsha, na kuchukia kuwanywesha watoto kabla yao, nikaendelea kusimama mpaka Alfajiri, ikiwa nililifanya hilo kwa ajili yako tuokoe, likafunguka kiasi kidogo cha kuiona mbingu.
Akasema mwengine: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na mtoto wa ‘ammi yangu nikimpenda sana kama vile mwanamume anavyokuwa na mapenzi kumpenda mwanamke. Nikamtaka akanikataa, mpaka siku alitaka dinaar mia, nikamkusanyia kwa taabu nikamletea, nilipotaka kumuingilia aliniambia: Muogope Allaah ewe mja wa Mungu usiivae pete isipokuwa kwa haki, nikainuka. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, wakafunguliwa. 

Akasema mwengine: Hakika mimi nilimuajiri mtu kwa kiasi cha kilo sita ya mchele malipo yake, alipomaliza kazi yake akasema: Nipe malipo yangu, nikampa malipo yake akayakataa, nikawa naikuza kiuchumi mpaka ikaleta faida ya ngo’mbe, akanijia akaniambia muogope Mola wala usinidhulumu haki yangu! Nikamwambia nenda kwa yule ngo’mbe, akaniambia muogope Mungu usinifanyie istihzai (shere), nikamwambia sikufanyii shere mchukue ngo’mbe. Akamchukua akaenda naye. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, likafunguka lote na wakatoka Akawaokoa Allaah. 

Amesema Wahab bin Manbah: Mfano wa yule anayeomba bila ya vitendo vyema ni kama mrushaji arushae chombo bila ya kamba. Akasema pia vitendo vyema huipeleka du’aa mbinguni. Kisha akasoma neno la Mola Aliyetukuka:
{{Kwake yeye yapanda kila maneno mazuri [mfano wa du’aa, tasbiih, adhkaar, usomi wa Qur-aan]; na vitendo vyema anavipokea, na kupata thawabu mtendaji.}}[Faatwir: 10] Amesema Qataadah: Hakubali Allaah neno ila kwa kitendo. 

5) Na katika sababu pia ni kuwafanyia wema na mazuri wazazi wawili. Lajulisha hilo kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiih yake kuwa: ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), alikuwa wamjiapo watu wa Yeman anawauliza je hapo kuna Uways bin ‘Aamir? Mpaka alipojiwa na Uways, akamwambia wewe ni Uways bin ‘Aamir, akasema ndio, unatoka Muraad kisha Qarn? Akasema ndio, akasema ulikuwa na mambalanga ukapoa isipokuwa sehemu kama mfano wa dirham? Akasema ndio, akasema una mama? Akasema ndio, akasema nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: 
((Atawajia nyinyi Uways bin ‘Aamir pamoja na watu wa Yeman, kutoka Muraad kisha Qarn, yeye ana mambalanga akapozwa na Allaah isipokuwa sehemu kama dirham, ana mama anamfanyia wema, lau atawaombea kwa Allaah atapokelewa du’aa yake, ukiweza akuombee msamaha lifanye hilo.))nikataka kuombewa msamaha akaniombea. 
Na Hadiyth iliyokuja katika Swahiyh Muslim katika Hadiyth ya watu wa Jabalini waliotajwa zamani, walikuwa kuna katika wao wanaojikaribisha kwa Allaah kwa wema wao wa wazazi wawili, ikawa ni sababu ya kujibiwa du’aa. 

6) Katika sababu za kujibiwa du’aa ni kumuombea mtu ndugu yake kwa siri. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiyh yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Du’aa ya mtu kumuombea ndugu yake kwa siri inajibiwa kupitia kwa Malaaikah aliowakilishwa kuwa kila amuombeapo ndugu yake kwa wema, mazuri, anasema Malaika: “Aamiyn nawe upate mfano wake”.))

Hadityh ni nyengine ni ile iliyopokewa na Abu Daawuud katika Sunan yake: Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Hakika du’aa inayojibiwa kwa wepesi, haraka ni ile inayoombwa kumuombea mtu kwa siri.))

7) Na du’aa katika safari hairudishwi kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Maombi matatu ni yenye kujibiwa, haina shaka ndani yake: Du’aa ya mwenye kudhulumiwa, du’aa ya msafiri na du’aa ya mzazi kwa mtoto wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Imekuwa du’aa ya msafiri ni yenye kukubaliwa, kwa kule kupata mashaka safarini, taabu na upungufu wa kila kitu akifanyacho kumfanyia Mola wake Aliye na cheo Mwenye nguvu.

8) Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni katika sababu za kujibiwa du’aa. Hili linathibitishwa kupitia Hadiyth ya Hudhayfah bin al-Yamaan kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Naapa kwa Yule nafsi yangu ipo mikononi mwake, mtaamrishana mema na kukatazana mabaya, ama atawaunganishia kwa kuwapa mfano wake Allaah na kuwateremshia nyinyi adhabu itokayo Kwake, kisha mumuombe Yeye na asiwajibu du’aa zenu.))[Imepokewa na at-Tirmidhiy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]

Imepokewa na Ahmad na al-Bazzaar kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 
((Enyi watu, hakika Mola Aliyetukuka Aliye juu Anawaambia nyinyi: Amrishaneni mema, na mukatazane mabaya kabla haijafikia kuniomba na nisiwajibu du’aa zenu, na mutake kwangu nisiwapatie, na mutake nusra kwangu nisiwanusuru.))

Amesema Ibnu Rajab katika Jaami’ul ‘Uluum Wal-Hikam “Hakika kufanya vitendo vilivyoharamishwa kwa kuendelea, kunazuia kujibiwa du’aa, na hivyo hivyo kuacha yaliyolazimishwa kama vile Hadiyth ilivyotuelekeza kuacha kuamrisha mema na kukataza mabaya ni sababu ya kuzuia kujibiwa du’aa, na yajulisha kufanya kila liloamrishwa inafanya du’aa kujibiwa.”

9) Na sababu ya kujibiwa du’aa ni kurudia Yaa RabbYaa Rabb. Nalo ni jambo kubwa linalotakiwa katika du’aa. Amesema Yaziyd Ruqashiy kutoka kwa Anas: “Hakuna mja yoyote atakaesema: Yaa RabbYaa RabbYaa Rabbisipokuwa  humwambia Mola wake nakuitikia, nakuitikia, nakuitikia.”

Imepokewa na Abu Dardaa na Ibnu ‘Abbaas kuwa wao wawili walikuwa wakisema: Jina kubwa la Allaah RabbRabb
Kutoka kwa Atwaa amesema: “Hatosema mja Yaa RabbYaa Rabb mara tatu, isipokuwa Mola humuangalia yeye, akasema je hamusomi Qur-aan? Kisha akasoma neno lake Mola Aliyetukuka:
{{Wale ambao wanamkumbuka kwa kumtaja Allaah wakiwa wamesimama, wameketi, wamelala kwa ubavu na wanafikiria uumbaji wa mbingu na ardhi wakasema: Ee Mola wetu hukuumba hizi bure bure umetakasika tukinge na adhabu ya moto.}} Mpaka katika neno lake: {{Akawajibu wao Mola wao: Hakika Yangu Mimi sipotezi kitendo cha mtendaji kati yenu.}} [Al-‘Imraan: 191- 195]

Amesema Ibnu Rajab na mwenye kuzingatia du’aa zilizotajwa katika Qur-aan, atazikuta du’aa nyingi zimeanza kwa jina la Rabbkama neno lake:
{{Na katika wao wanaosema Mola wetu, tupe sisi katika dunia mema na Akhera mema na utukinge na adhabu ya moto.}} [Al-Baqarah: 201] 
Na neno Lake:
{{Mola wetu usizigeuze kwa kuzipoteza nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na tupe sisi rahmah itokayo Kwako, hakika Yako Wewe ni mwema kwa kutoa.}}[Al-‘Imraan: 8]

10) Na pia imepokewa na AbU Dunya katika kitabu cha Mujaabiyna Fiy Du’aakutoka kwa Hasan amesema: “Alikuwa mtu katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Answaar amebandikwa jina la Aba Mu-uliq. Alikuwa mfanyabiashara kwa mali yake na wengine akienda nao safarini alikuwa akiinamisha kichwa kwa uchaji Mungu. Siku moja alitoka akakutana na mwizi aliyebeba silaha, akamwambia: Toa ulicho nacho, nitapigana na wewe, akamwambia kwanini waitaka damu yangu? Unalolitaka ni mali, akasema ama mali ni yangu sitaki ila damu yako, akamwambia ikiwa hilo ni lengo lako niwache niswali rakaa nne, akamwambia swali ikiwa huna budi kufanya hilo, akatawadha akaswali rakaa nne, akasema katika sijdah yake ya mwisho kwa kuomba: “Ee Mwenye mapenzi, Mwenye kiti cha enzi, Mtendaji kwa ulitakalo, nakuomba kwa cheo Chako kisichomalizika, na ufalme Wako usio na dhulma, na mwangaza wako uliojaa nguzo za ‘Arshi Yako, unikinge na shari ya mwizi huyu, ewe Msaidizi nisaidie, ewe Msaidizi nisaidie, akasema mara tatu, akatokea mpanda farasi amebeba silaha za vita ameziweka katika farasi wake, alipomuona mwizi alimuelekea akamchoma (akamdunga) na akamuua.

Kisha akamuendea akamwambia inuka. Akamuuliza wewe ni nani, hakika Ameniokoa Allaah kwa njia yako leo. Akamwambia mimi ni Malaika wa mbingu ya nne uliomba kwa du’aa yako ikagonga mlango wa mbinguni kwa mshindo wake, kisha ukaomba mara ya pili ikasikika vilio vya watu wa mbinguni, kisha uka omba mara ya tatu, nikaambiwa du’aa ya mwenye dhiki. Nikamuomba Allaah Anipe mimi uwezo wa kumuua. Amesema Hasan: “Mwenye kutawadha akasali rakaa nne na akaomba kwa du’aa hii atajibiwa du’aa yake, mwenye dhiki ama awe hana dhiki (shida).”

11) Na katika sababu za kujibiwa du’aa ni kuchunguza (kujua) wakati wa kujibiwa, na kuwa mnyenyekevu kwa Allaah Aliyetukuka na kuulinganisha moyo wako unapoomba du’aa - uwe moyo wako upo hapo.
Amesema Ibnu Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu cha Jawaabul-Kaafiy  “Yatakapoungana mambo mawili  kwa muombaji - kuuhudhurisha moyo wake na kupata wakati wa kujibiwa katika wakati sita nao; - thuluth ya mwisho ya usiku, na wakati kunapoadhiniwa, na baina ya adhaan na iqaamah, na mwisho wa kila Swalah tano za faradhi, na apandapo Imaam katika mimbari siku ya Ijumaa mpaka Swalah imalize kuswaliwa, na saa ya mwisho baada ya alaasiri siku ya Ijumaa, na ikapatikana unyenyekevu moyoni  na kujiweka chini mbele ya Mola wake, na kuwa mnyonge, dhaifu, kujielekeza kwa Mola,  na kuelekea Qiblah, na akawa ametawadha (yuko twahara), na akainua mikono yake kwa Mola wake, na akaanza kumshukuru Mola na kumsifu, kisha akafuatiliza kumswalia Muhammad mja Wake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akazitanguliza haja zake, kwa kutubia na kuomba msamaha, kisha akajilazimisha katika kuomba, kwa kujipendekeza kwa Mola wake, katika du’aa zake kwa kuwa na hima na hicho, kwa kuziunganisha kwa majina ya Mola, na sifa Zake, pamoja na kumpwekesha, na akawa du’aa  zake anazifuatanisha na Swadaqah, hakika du’aa hii haitokuwa ni yenye kurudishwa kabisa.

Na swalaah na salaam zimfikie Mtume wetu Muhammad na aali zake na Maswahaba zake na amani.


SAYDINA ABUBAKAR


Abu Bakr  رضي الله عنه  Na Sababu Za Kupewa Cheo Cha  'As-Swiddiyq' (Msema Kweli)

Al-Imaam An-Nawawiy amesema: "Ummah umekubaliana kwa pamoja bila ya kupingana kwamba amepewa cheo cha 'As-Swiddiyq' kutokana na kuitikia kwake haraka kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  bila ya kusita na kukubali maneno yake kwamba daima ni ya ukweli. Alibakia kuwa mkweli maishani mwake kote wala hajapata kusema uongo  hata mara moja". 
Ibn Kathiyr amesema: "Kuhusu cheo chake cha  'As-Swiddiyq', inasemekana kwamba alipewa tokea zama za Ujaahiliyyah kutokana na ukweli uliojulikana kwamba alikuwa ni mkweli. Vile vile imesemekana kwamba amepewa cheo hicho kwa sababu alikuwa daima yuko tayari kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلمkatika kila jambo alilosema".
Baadhi ya matukio yaliyodhihirisha ukweli wake na wepesi wake wa kuamini lolote alilosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
1.    Katika kisa cha Israa Wal-Mi'raaj alipobakia kuwa thabiti na kuwaambia makafiri kwamba ikiwa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم  mwenyewe ametamka maelezo hayo basi ni kweli!
Ibn Kathiyr amesema: "Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah wamesema: "Alijulikana kwa mara ya kwanza kwa cheo hiki asubuhi ya siku ya tukio la Israa". Al-Haakim amesimulia kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها  ambaye amesema: Washirikina walikuja kwa Abu Bakr wakamwambia: "Umemsikia rafiki yako anavyodai? Anadai kwamba amesafiri kwenda Baytul-Maqdis kwa usiku mmoja" Akauliza: "Je, amesema mwenyewe hivyo?". Wakajibu: "Ndio". Akasema: "Basi amesema ukweli! Naamini ukweli wake katika mambo yaliyo ya ajabu zaidi kuliko hayo, kama 'habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni" (yaani wahyi wa Qur-aan). Tokea hapo Abu Bakr akapewa cheo cha 'As-Swiddiyq'.  [Ibn Kathiyr kasema Isnaad yake ni nzuri]. 
Al-Haakim amesimulia kutoka Nazaal ibn Swabrah ambaye amesema: "Tulimwambia 'Aliy: "Ewe kamanda wa waumini! Tuelezee kuhusu Abu Bakr". Akasema: "Ni mtu aliyepewa jina la 'As-Swiddiyq' na Allaah سبحانه وتعالى kwa kauli ya Jibriyl عليه السلام na kauli ya Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم . Alikuwa ni Khalifa  wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliridhika naye katika dini yetu na aliridhika naye katika mambo yetu ya kidunia".  [Ibn Kathiyr kasema: Isnaad yake ni nzuri] 
Na katika Hadiyth ya vita vya Uhud, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliliambia jabali        la Uhud lilipotikisika (kwa kulipapasa)
((أثبت أحد فإنما عليك نبي وصديق وشهيدان))
((Tulia kwani juu yako yumo Mtume, As-Swiddiyq na mashahidi wawili))(yaani ‘Umar na ‘Uthmaan رضي الله عنهم) [Al-Bukhaariy]
2.    Kuhama (Hijrah) kwake na Mtume صلى الله عليه وآله وسلمakiwa ameacha familia yake ili abakie na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم . Maswahaba wote waliruhusiwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhama (Hijrah kutoka Makkah kwenda Madiynah) isipokuwa Abu Bakr. Mtume صلى الله عليه وآله وسلمalikuwa akimwambia abakie ili awe swahib (rafiki) yake katika Hijrah na Allaah سبحانه وتعالىAkatimiza pendekezo la Mjume Wake  صلى الله عليه وآله وسلم .  Kisha yaliyotokea walipokimbilia katika pango la At-Thawr na   Aayah iliyoteremeshwa kuelezea hivyo:
  ((إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُواْ ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ
 إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ 
لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُواْ السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ))
((Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allah  Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia swahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allah Yu pamoja nasi. Allah Akamteremshia utulivu wake, na Akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na Akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allah kuwa ndilo juu. Na Allah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima)) [At-Tawbah:40
3.    Alipolia wakati Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisema: ((Hakika kuna mja alipewa uchaguzi na Allaah سبحانه وتعالى   baina ya Duniya na Akhera, mja akachagua Akhera)). Abu Bakr alijua kuwa huyo mja ni Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na alitambua kauli hiyo imemaanisha kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ataaga duniya karibuni. [Al-Bukhaariy]
4.    Alipobakia kuwa thabiti katika kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wakati Maswahaba waliduwaa hawakujua la kufanya na khutbah yake aliyotoa ya kuwatuliza.
5.    Kuthibitika kwake ingawa alikuwa pekee katika kupeleka jeshi na    kumfanya Usaamah bin Zayd awe mwenye kuongoza jeshi.
6.    Kung'ang’ania kwake katika kupigana na watu waliotoka nje ya Uislam baada ya kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
7.    Alipomchagua 'Umar bnul-Khattwaab رضي الله عنه kuwa Khaliyfah wa Waislam, lilikuwa ni chaguo tukufu lililokubalika na Ummah na ni jambo ambalo limeainishwa na Maulamaa kuwa ni jambo mojawapo muhimu la mafanikio katika historia.

SHEIKH SHARIF YUSSUF

HASAD KATIKA NDOA 1

HASAD KATIKA NDOA:  Baadhi ya watu hufanya chuki ama husda katika ndoa za watu kwa kutumia vitu mbalimbali, ikiwa kwa kusambaza maneno ya k...